Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Tanzania Salim Hassan Turky akimkabidhi sehemu ya madeski hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya kuchangia madeski Zanzibar Haroun Ali Suleiman Bandarini Zanzibar.
Wafanyakazi wa bandari ya Zanzibar wakishusha madeski yaliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya wanafunzi wa Zanzibar
…………………………………………………………………………………………………………
Na Mwashungi Tahir -Maelezo Zanzibar
Jumla ya madawati 5,500 ikiwa ni mgao wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yamewasili Zanzibar kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wa skuli za Unguja na Pemba.
Akipokea madawati hayo bandarini Zanzibar, Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya madawati Zanzibar Harou n Ali Suleiman alisema mgao huo utapunguza tatizo kubwa la madawati linalozikabili skuli nyingi hapa nchini.
Alisema kupatikana kwa madawati hayo kutaleta faraja kwa wanafunzi na kuongeza hamasa na ari katika kujipatia elimu.
“Msaada huu utapunguza usumbufu wa wanafunzi kukaa chini kwa muda mrefu na utaongeza ufanisi kwa walimu na wanafunzi katika kusomesha na kujifunza, “alisema Mwenyekiti huyo.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma aliwashukuru Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia kupatikana madawati hayo na ameeleza matumaini yake ya kupatikana msaada zaidi wa madeski.
Amewaomba wasamaria wema kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na tatizo la madawati kwa kutoa michango yao kupitia Kamati ya Taifa ya Madawati ya Zanzibar.
Aidha amewaomba walimu wakuu wa skuli zitakazopata madeski hayo kuwapa elimu wanafunzi jinsi ya kuyatunza ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Sambamba na hayo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zuberi Ali Maulid alisema kupatikana kwa madeski hayo ni faraja kwa baraza hilo kwani suala hilo linazungumzwa sana na tumeanza kuona mafanikio yake.
Alisema kupatikana kwa msaada huo ni jambo la kupigiwa mfano kwa wabunge kwani wabunge waliopita hawajawahi kufanya jambo kama hilo.
Makamo Mwenyekiti wa wa Bunge Salim Hassan Turky ambae ni Mbunge wa Jimbo la Mpendae kwa niaba ya wabunge wenziwe amesema madawati hayo ni mchango wa bunge uliotokana na pesa za bajeti zilizobakia katika bajeti iliyopita.
Jumla ya shilingi billion sita zimetumika kununulia madawati hayo ambayo ni kila jimbo lilitarajiwa kupata madeski 300 na kwa kuanzia kila jimbo limetapatiwa madeski 100 na mengine yatafuatia baadae.
Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano Mh. John Pombe Magufuli kwa kutoa wazo la kutumia fedha zilizobaki za bunge bajeti iliyopita kwa kununulia madeski hayo.
No comments:
Post a Comment