Waziri mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameagiza wakuu wa wilaya na mikoa kufanya ziara katika maeneo yao hasa vijijini ili kujua matatizo ya wananchi wao kwa ukaribu na kuyapatia ufumbuzi.
Mhe.Majaliwa ameyasema hayo leo hii Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wakuu wa wilaya na mikoa walipokuwa Ikulu wakila kiapo cha maadili ya viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na wakuu wa mikoa yao.
Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa wakuu wa mikoa na wilaya waache kukaa maofisini mwao badala yake watembelee wananchi na hasa wale wa hali ya chini ili kujua matatizo yao ya Ardhi na kupatia ufumbuzi migogoro ya wafugaji na wakulima.
Pia Mhe.Majaliwa amewasisitiza wakuu hao kutambua kwamba majukumu waliyonayo ni makubwa na wananchi wana mategemeo makubwa juu yao na hivyo ni budi wakatekeleza wajibu wao na kuhakikisha watanzania wanapata huduma zote za muhimu kwa kutumia elimu, uwezo, uadilifu, uaminifu na uwajibikaji walionao ili kufanikisha maendeleo kwa wananchi.
Aliongeza kuwa wakuu hao wana jukumu kubwa la kusimamia pesa za serikali pesa za miradi zinakokwenda katika halmashauri za wilaya zao na kukazia kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote ambaye hatofanya kazi zake kikamilifu.
Waziri mkuu amewaagiza wakuu wa Mikoa kushirikiana kwa karibu na wakuu wa Wilaya ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya maeneo yao kwani wananchi wana kiu ya maendeleo katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment