Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wanawake TAWLA Ms. Aisha Zumo Bade akisoma hotuba yake waakati wa wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Chama hicho unaofanyika kwenye hoteli ya Hyyat Regency jijini Dar es salaam leo.
Mtoa Mada Agustus Emmanuel Fungo akiwasilisha mada ya masuala ya kiuchumi kwa wanasheria wa Chama cha wanasheria wanawake TAWLA wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika Hyyat Regency jijini Dar es salaam leo.
Mtoa Mada Dr. Elie Waminian Akizungumza wakati akitoa mada wanawake kujiamini katika maisha yao ikiwa ni pamoja na kutokuwa wavivu.
Baadhi ya wanasheria wanawake walioshiriki katika mkutano huo wakifurahia mada zilizokuwa zikitolewa.
Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wanasheria wanawake Tike Mwambipile akihojiwa na waandishi wa habari wakati wa mkutano hu.
Baadhi ya majaji na wanasheria wakishiriki katika mkutano huo.
Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Wanawake wametakiwa kushiriki shughuli za kiuchumi ili kujikomboa na kukandamizwa na mifumo ya kijamii iliyopo sasa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria Wanawake nchini (TAWLA), Bi Tike Mwambipile leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa chama hicho.
Bi Mwambipile amesema kuwa wanawake wa Kitanzania wananyanyasisika sana kwani hawana vipato vya kutosha, hivyo inabidi waongeze juhudi katika kuibua na kubuni miradi endelevu ya ujasiriamali ili kukuza vipato vyao.
“Wanawake mnapaswa kujiunga na VICOBA na Saccos ili muweze kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kufanyia biashara,”alisema Bi Mwambipile akiongeza kuwa kipato kinachopatikana inabidi wanawake wawe na maamuzi ya kukitumia bila kusubiria maelekezo ya waume zao.
Naye Mwenyekiti wa TAWLA, Bi Asia Bade amesema kuwa wakati umefika kwa wanawake kujitambua kuwa ni sehemu muhimu katika jamii hivyo kutumia uwezo wao kujikwamua kiuchumi pasipo kutegemea wanaume.
Bi Bade ameongeza kuwa suala la ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za kiuchumi litawakomboa na utumwa wa kipato ambao umewatesa kwa kipindi kirefu.
Kwa upande wake mjumbe wa Mkutano huo, Dkt. Pindi Chana ameishauri Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuweka sharti la mkakati wa kuwainua wanawake na vijana kwenye mabenki yanayoomba usajili. Ameongeza kuwa bila kuonyesha makakati huo, BOT isitoe kibali kwa benki yoyote.
Dkt. Chana ameonyesha kukerwa na riba za mikopo kuwa juu sana kwa wakopaji na kusema, “Watanzania tunayafanyia mabenki kazi kutokana na riba kubwa wanazotuwekea kwenye mikopo, hii haitunufaishi bali inatutesa katika kurejesha.”
Akionyesha kukerwa na utegemezi wa wanawake, Mjumbe wa Mkutano huo, wakili Mary Kessy amesema ni wakati wa wanawake kuacha kubweteka wakisubiri kupokea kutoka kwa waume zao bali wachangamkie fursa zilizopo ili wawe na kipato cha uhakika.
Bi Kessy amesema kwamba kuna fursa nyingi za kuwainua wanawake kiuchumi ambazo ni pamoja na ushiriki katika shughuli za madini, kilimo, mifugo na uvuvi pia kutumia mabenki ya wanawake.
“Huu sio wakati wa kuchagua kazi, wanawake tujitume, fursa ziko nyingi sana hapaTanzania, kama ni kwenye migodi tuwemo, biashara za kimataifa tufanye na kwenye nafasi za uongozi tujitokeze badala ya kulalamika” amesisitiza Bi Kessy.
Huu ni Mkutano wa 25 ambao unawajumuisha wanawake wanasheria nchini kuweza kubainisha namna ya ushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuweka mikakati ya kutoa elimu endelevu ya uzalishaji mali.