Msemajiwa Chama cha Mapinduzi CCM Christopher Ole Sendeka akizungumza na waandishi wa habari leo katika Makao Makuu Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba kushoto ni Mkuu wa Utawala Makao Makuu Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba Bakari Hamis.
……………………………………………………………………………………………………..
Jana tarehe 27/7/2016 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walitoa kauli kwa Waandishi wa Habari kupitia Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Ndugu Freeman Mbowe (Mb). Tamko hilo kama ilivyo kawaida ya CHADEMA lilijaa uongo mwingi na ghiliba nyingi za kibabaishaji na kuthibitisha ukweli kuwa kwa hakika kutokana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dr. John Pombe Magufuli wapinzani nchi hii wamekosa ajenda na hivyo njia peke yake wanayoona inafaa ili waendelee kufanya utapeli ni kutunga uongo, kujiaminisha katika uongo huo na kuusambaza uongo huo ili kujaribu kupata wafuasi.
Katika uongo na uzushi huo walioutangaza jana, CHADEMA wanasema wameamua kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa tarehe waliyoitaja na maandamano hayo yatafanyika chini ya operesheni waliyoiita UKUTA. Kimsingi hoja walizozitumia kufikia uamuzi wao bila kuzirudia zimejaa upotoshaji na uongo uliokithiri. Kwa mfano wanadai Serikali imezuia mikutano yote ya vyama vya siasa, huku wakijua kuwa ni uongo kwani Serikali haijazuia mikutano kwenye majimbo yao, Wabunge wako huru kufanya shughuli zao kwenye majimbo yao, na tumeona Wabunge wakifanya shughuli zao majimboni bila shida wakiwemo hao wa vyama vya upinzani.
Lakini vyama vya siasa kufanya shughuli kwa mujibu wa katiba ya vyama vyao sio jambo lililozuiliwa pia, ndiyo maana tumeshuhudia vyama vikifanya mikutano yao ya kikatiba bila tabu.
Lakini mfano mwingine wa hoja za uongo na uzushi, ni hoja eti ya Serikali hii ya Awamu ya Tano kuwa ya kidikteta. Udikteta hasa unaosemwa na Chadema ni upi? Ni huu wa kushughulikia watumishi hewa? Ni huu wa kuwabana wakwepa kodi? Ni huu wa kupunguza na kudhibiti safari za nje? Ni huu wa kubana matumizi ya Serikali? Ni huu wa kufukuza wabadhirifu na wazembe kazini? Hivi udikteta huo ni huu wa kushughulikia mafisadi mpaka kuanzisha mahakama yao? CCM inaamini Watanzania walio wengi wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli na Serikali yake, sasa kama kwa Chadema hatua hizi ndiyo tafsiri yake ni udikteta basi bila shaka wao ni sehemu ya mfumo mbovu ndiyo maana wako tayari kuleta vurugu ili wautetee.
Kwa kuwa CHADEMA wamezoea kujenga Chama chao kwa harakati zinazohusisha kumwaga damu za Watanzania wasiokuwa na hatia, ukweli huu wa maelekezo ya Serikali hawausemi, isipokuwa wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha wanafanya mambo ambayo mwisho wa siku yatasababisha vurugu, uvunjifu wa amani na umwagaji damu.
Lakini pengine ni muhimu Watanzania na wapenda amani nchini na duniani wakajiuliza ni kweli kuwa lengo la hizi vurugu na maandamano haya ni la kujenga na si kubomoa? Kwa nini kila operesheni ikifanywa na CHADEMA huwa inaambatana na umwagikaji wa damu za Watanzania wasiokuwa na hatia? Wakati wa Maandamano hayo inapotokea madhara ni kwa nini waathirika huwa sio viongozi waanzilishi wa maandamano hayo wala wake au waume zao au watoto wao au hata ndugu zao wa karibu bali huwa ni watu wengine nje ya hao ndugu zao wa karibu? Mpaka lini damu za Watanzania wasio na hatia zitaendelea kutumika kutafuta umaarufu wa CHADEMA na viongozi wake?
Hii ni kwa faida ya nani hasa? Kwa nini pamoja na kuelekezwa namna bora ya kufanya siasa wao huwa hawataki kufuata utaratibu? Hivi ni kweli kuwa hawajui bila kufuata utaratibu jambo lolote huwa ni vurugu?
Chama Cha Mapinduzi kinapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa ni vizuri kutafakari na kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kuamua kushiriki au kuruhusu watoto wetu kwenda kuwa kafara ya walafi wachache wa madaraka. Ni vizuri tukayakumbuka matukio kwenye operesheni kama hizi yaliyopoteza maisha ya vijana wetu na matokeo ya kila operesheni.
Pamoja na ukweli kuwa hakuna operesheni yeyote kati ya zote zilizowahi kufanywa na Chadema ambayo imewahi kuwasaidia Watanzania wa kawaida zaidi ya kujenga umaarufu wa viongozi wachache wa Chadema na kuneemesha matumbo yao na ya familia zao, operesheni zote zimepoteza maisha ya Watanzania kadhaa wasiokuwa na hatia wala wasiofaidika kwa lolote na operesheni hizo.
Kama nia ni njema kwa nini hawataki kufuata Sheria na taratibu tulizojiwekea? Demokrasia gani isiyokuwa na mipaka? Demokrasia bila mipaka ni fujo. Tunaomba vyombo vinavyohusika visisite kuchukua hatua zinazostahili bila kumuonea mtu lakini bila kufumbia macho vitendo vyenye lengo la kuwahujumu Watanzania waliowengi walioamua kuchapa kazi kuitikia wito wa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya kazi.
Lakini pia tunawashauri Watanzania, wapenda amani, utulivu na maendeleo kupuuza wito wa vurugu na uvunjifu wa amani badala yake wajikite kwenye kuchapa kazi na kujitafutia maendeleo yao kwa kufanya kazi kwa bidii.
Maendeleo hayaji kwa maandamano, maendeleo huja kwa kuchapa kazi kwa bidii. Maendeleo hayaji kwa vurugu na fujo nchini, bali amani na utulivu ni vichocheo muhimu vya maendeleo ya kweli.
Imetolewa na:-
Christopher Ole Sendeka (MNEC),
MSEMAJI WA CHAMA
28/07/2016