Tuesday, 12 July 2016

NEW UGANDA:Museveni atuma jeshi kuokoa waganda Sudan Kusini



Uganda imeanza mikakati ya kuwaondoa raia wake nchini Sudan Kusini baada ya machafuko yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu mia mbili na sabini.
Rais Yoweri Museveni alikuwa ametoa agizo kwa jeshi la taifa UPDF kwenda Sudan Kusini kuwaokoa raia wake walioko huko.
Msemaji wa jeshi Paddy Ankunda amenukuliwa akithibitisha kuwa kikosi kidogo cha wanajeshi kitakwenda kwa barabara kuwaokoa waganda walioathirika na mapigano.
Bwana Ofwono Opondo naye aliongezea kusema kuwa
“Rais Museveni ameamuru majeshi ya UPDF kuwaokoa waganda walioko Nisitu, Mashariki mwa mto Nile S.Sudan.”
Hatua hiyo ilifuatia ripoti ya mauaji ya wafanya biashara watano raia wa Uganda miongoni mwa watu zaidi ya 272 waliouawa majeshi watiifu kwa rais Salva Kiir walipokabiliana vikali na wanajeshi watiifu kwa makamu wa rais wa Sudan Kusini bw Riek Machar mjini Juba.
Hayo yanajiri huku Uwanja wa ndege mjini Juba ukifunguliwa baada ya kufungwa kutokana na mapigano hayo.
Tayari mataifa kadhaa yametangaza kutuma ndege kuwachukua raia wao waliokwama Sudan Kusini.
Kenya imetangaza kutuma ndege ili kuwahamisha raia wake.
Licha ya hali ya utulivu kushuhudia hii leo, bado kungali na hofu ya mapigano mapya kuzuka.
Watu wachache wameonekana wakienda madukani kutafuta bidhaa muhimu.
Mashirika ya misaada yanasema hakuna maji safi ya kunywa na mahitaji muhimu.
Mji wa Juba hutegemea maji yanayosambazwa kwa matrela kwani hakuna mabomba ya maji.
Umoja wa mataifa unasema karibu watu elfu 40 wamekimbia mapigano ya karibuni, lakini huenda idadi hiyo ikawa kubwa zaidi.
Kwa sasa mustakabali wa taifa hili changa zaidi la Afrika haujulikani, matumaini yakiwa katika kutekelezwa kwa mkataba wa amani wa mwaka uliopita.


No comments:

Post a Comment