Tuesday, 12 July 2016

Chama Cha Kuogelea chapongeza semina ya Dar Swim Club

Chama cha mchezo wa kuogelea nchini (TSA) kimeipongeza klabu ya Dar Swim Club (DSC) kwa kufanya semina ya kuendeleza mchezo huo kwa wachezaji na makocha iliyokuwa chini ya wakufunzi kutoka klabu ya Hamilton Aquatics ya Dubai.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhan Namkoveka mara baada ya kutembelea mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye bwawa la kuogelea la shule ya kimataifa ya DIA iliyopo Masaki jijini.

Mafunzo hayo yalikuwa chini ya wakufunzi wa kimataifa wa mchezo wa kuogelea wa klabu bingwa ya Mashariki ya Kati (Middle East) ijulikanayo kwa jina la Hamilton Aquatics ya Dubai, Nebojsa Durkin na Katy Morris.

Mafunzo hayo yalidhaminiwa na kampuni za Alios Finance Tanzania, Europcar, DSC, DIA na kampuni ya utafiti na uchimbaji wa mafuta ya Maurel & Prom.

Wakufunzi hao walifuraishwa na viwango vya waogeleaji wa klabu hiyo pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali za mchezo huo ikiwa pamoja na kukosa bwawa la mita 50 linalotambuliwa kimataifa.

Namkoveka alisema kuwa wamefuraishwa na mafunzo hayo ambayo yaliwahusisha waogeleaji chipukizi (yoso) na wakubwa pia na makocha wa timu hiyo. Alisema kuwa wamevutiwa na jinsi mafunzo hayo yalivyokuwa yanaendeshwa na anaamini Tanzania itapata waogeleaji nyota kama wadau wa mchezo huo wataiga mfano wa DSC.
Kocha wa timu ya DarSwim Club, Radhia Gereza (kulia) na Salum Mapunda (kushoto) wakiwaelekeza waogeaji watoto wa klabu ya Dar Swim Club baada ya kupata mafunzo kutoka kwa wakufunzi wa klabu ya Hamiton Aquatics ya Dubai.

“Nimefuraishwa na jinsi mafunzo yalivyoendeshwa, kwa kweli nimevutiwa sana kwani nimeona jinsi waogeleaji chipukizi waliokuwa wanaanza kujifunza mchezo, waogeleaji wenye uelewa wa mchezo na makocha walivyokuwa wanapewa mafunzo, hii ndiyo njia sahihi ya kuendeleza mchezo huu,”

“Naamini, kama juhudi hizi zitaendelezwa, Tanzania itakuwa na waogeleaji wengi wenye ubora wa kimataifa katika miaka ijayo, mchezo wetu unahitaji sapoti kubwa sana ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea,” alisema Namkoveka. Kocha wa Dar Swim Club, Michael Livingstone alisema kuwa wamepata mwanga mkubwa katika mafunzo hayo ambayo watayatumia katika kuendeleza mchezo katika klabu yao na kwa Taifa kwa ujumla.

“Tumejifunza mbinu, ujuzi na mambo kadha wa kadha kuhusiana na mchezo wa kuogelea, kwa kifupi tumepata mwanga wa hali ya juu kwa ajili ya ufundishaji kwa waogeleaji yoso na wakubwa,” alisema.

Katibu Mkuu wa DSC, Inviolata Itatiro amesema kuwa wamepania kuweka historia nchini kwa kutoa waogeleaji bora na ndiyo maana waliamua kuendesha mafunzo hayo yaliyokuwa yanafanyika kwa mara ya pili.

“Tunahitaji sapoti katika mchezo huu, lengo ni kuona waogeleaji wanapata maendeleo makubwa kwa kufikia viwango, nawaopongeza wadhamini Alios Finance Tanzania, Europcar, DSC, DIA na kampuni ya utafiti na uchimbaji wa mafuta ya Maurel & Prom kwa kutuunga mkono, gharama za kuwaleta walimu kutoka nje ni kubwa sana,” alisema Inviolata. Mwisho….
Mafunzo ya kuogelea siyo lazima yafanyikie kwenye maji. Hapa mkufunzi wa kimataifa wa mchezo wa kuogelea kutoka klabu ya Hamilton Aquatics, Nebojsa Durkin aionyesha kwa vitengo waogeleaji wa Dar Swim Club jinsi ya kuchumpa kwenye maji (ku-dive) katika mafunzo yaliyomalizika hivi karibuni kwenye shule ya Kimataifa ya DIA, Masaki.
Mkufunzi wa kimataifa wa mchezo wa kuogelea kutoka klabu ya Hamilton Aquatics ya Dubai, Nebojsa Durkin aionyesha kwa vitengo waogeleaji wa Dar Swim Club jinsi ya kugeuka kwa kasi kwa kutumia nguvu ya miguu katika mafunzo yaliyomalizika hivi karibuni kwenye shule ya Kimataifa ya DIA, Masaki.
Mkufunzi wa kimataifa wa mchezo wa kuogelea kutoka klabu ya Hamilton Aquatics ya Dubai, Katty Morris akielekeza jinsi gani ya kuchumpa (ku-dive) kwa umbali mrefu na kwa malengo maalum kwa waogeleaji wa Dar Swim Club katika mafunzo yaliyomalizika hivi karibuni kwenye shule ya Kimataifa ya DIA, Masaki.
Hapa sasa ni Kazi Tu: Kocha wa Dar Swim Club, Michael Livingstone akiwafanyika mazoezi ya kuchumpa (ku-dive) waogeleaji wa klabu hiyo. Waogeleaji hao walifanya tendo hilo kwa staili mbalimbali baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa makocha wa klabu maarufu ya Hamilton Aquatics, Nebojsa Durkin na Katy Morris.
Kocha wa Dar Swim Club, Salum Mapunda akiwasimamia waogeaji yoso wa klabu ya hiyo katika mafunzo hayo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Kuogelea (TSA) Ramadhan Namkoveka (wa tatu kutoka kushoto) na Mkurugenzi wa Ufundi Amina Mfaume (wa tatu kutokakulia) wakiwa ktika picha ya pamoja na wakufunzi wa mchezo huo kutoka Dubai, Nebojsa Durkin (wa pili kushoto), Katy Morris (wa nne kutoka kushoto) na viongozi na makocha na viongozi wa klabu maarufu ya Dar Swim Club, Kocha Kanisi Mabena (wa kwanza kushoto), Michael Livingstone (wa pili kulia) na Katibu Mkuu wa klabu hiyo Inviolata "Iron Lady" Itatiro wa kwanza kulia.

No comments:

Post a Comment