Tuesday, 19 July 2016

NEW NYAMONGO REFORM IN TARIME:Wananchi wakubali mapendekezo ya utatuzi Mgogoro wa Nyamongo

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza wakati wa Kikao cha kujadili taarifa ya Kamati iliyoundwa na Profesa Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo, kilichofanyika wilayani Tarime. Kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na wa Pili kushoto ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.
Baadhi ya wananchi wilayani Tarime, wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) wakati wa Kikao cha kujadili taarifa ya Kamati iliyoundwa na Profesa Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo, kilichofanyika wilayani Tarime.
Wajumbe wa Kamati iliyoundwa na Profesa Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo, wakiwa katika kikao cha kujadili taarifa ya Kamati hiyo, kilichofanyika wilayani Tarime.
Katibu wa Kamati iliyokuwa kutathmini migogoro kati ya Mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo, Mhandisi John Shija kutoka Wizara ya Nishati na Madini, akisoma taarifa ya Kamati hiyo mbele ya wananchi na viongozi mbalimbali wilayani Tarime. Kushoto kwake ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje na kulia kwake ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi, Mhandisi Juma Sementa.

Na Teresia Mhagama

Wananchi mbalimbali wilayani Tarime wamekubali mapendekezo yaliyotolewa na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Hayo yalibainika wakati wa Kikao kilichokuwa kikijadili taarifa ya Kamati hiyo kilichofanyika wilayani Tarime, kikiongozwa na Waziri wa Nishati na Madini na kuhudhuriwa na baadhi ya wananchi, Madiwani, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime Vijijini, watendaji wa Mgodi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya na Kamati iliyokuwa ikitathmini kero hizo.

Profesa Muhongo alisema kuwa Mapendekezo hayo ya Kamati yalipatikana baada ya kuhoji wananchi 4,400 kutoka vitongoji 80 vya Halmashauri husika huku hadidu za rejea zikiwa 16.

“Mapendekezo yote mliyoyatoa yamekubaliwa sasa kinachofuata ni nyinyi Kamati kupita katika kila kitongoji na kuwaeleza wananchi kuhusu maamuzi yaliyofikiwa mkizingatia pia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa katika kikao hiki na Wawakilishi wa wananchi kama Mbunge na Madiwani,” alisema Profesa Muhongo.

Awali Katibu wa Kamati hiyo, Mhandisi John Shija kutoka Wizara ya Nishati na Madini, alisema kuwa Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 27 ambapo wataalam wa Serikali walikuwa 19, wawakilishi wa mgodi 4 na wawakilishi wa wananchi kupitia Ofisi ya Mbunge wa Tarime vijijini wakiwa 4.

Mhandisi Shija alisema kuwa Kamati ilipewa hadidu za rejea 16 ambapo baadhi ya hadidu hizo zinahusu masuala ya fidia ya ardhi, athari za mgodi kwa mazingira, binadamu na mifugo, uvamizi wa mgodi unaofanywa na vijana, askari wanaolinda mgodi kunyanyasa wananchi na wachimbaji wadogo kupatiwa maeneo ya kuchimba madini.

“Katika kuyachunguza masuala yaliyomo kwenye hadidu za rejea, Kamati ilipitia taarifa mbalimbali na kuwahoji wananchi, pia ilikutana na viongozi wa mgodi wa NorthMara, Wilaya, Watendaji wa Halmashauri, Kata, Vijiji na kukagua shughuli za Mgodi na maeneo yanayozunguka Mgodi,”alisema Mhandisi Shija.

kuhusu maeneo ambayo Mgodi uliwaambia wananchi wasiyaendeleze huku maeneo hayo yakifyekwa wakati wa uthamini, Kamati ilipendekeza kuwa Mgodi ulipe fidia ya mazao yaliyofyekwa na fidia ya usumbufu. “ Kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, fidia ya usumbufu ni asilimia 8 ya fidia kuu (Fidia ya mazao), Kamati inapendekeza mgodi ulipe fidia hiyo kwa kiwango cha asilimia 50 badala ya Nane,” alisema mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo.

Kuhusu wananchi ambao walikataa kufanyiwa uthamini katika maeneo ya MjiniKati na Nyabichune wilayani Tarime, Kamati ilipendekeza kuwa mgodi ufanye tathmini ndani ya wiki Tatu kwa mujibu wa hali ya mwaka 2012, na wananchi hao wakiendelea kukataa, Serikali itawafanyia uthamini na kuutaka Mgodi uwalipe kwa mujibu wa viwango vya serikali.

Aidha kuhusu suala la wananchi kujenga katika eneo la Mgodi kwa lengo la kujipatia faida, Kamati ilipendekeza kuwa wananchi hao wasilipwe chochote kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria ambapo Kamati iliasa Mamlaka husika kuendelea kusimamia sheria ili masuala hayo yasiendelee kujitokeza.

Vilevile kuhusu madhara waliyopata wananchi kutokana na shughuli za mgodi kama vile milipuko, vumbi, maji, na mifugo kufa kwa madai ya maji yaliyochafuliwa kutokana na shughuli za mgodi, Kamati ilipendekeza kuwa malalamiko yenye ushahidi yapelekwe mgodini ili yafanyiwe kazi ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia zao na ikishindikana yapelekwe kwa Kamishna wa Madini.

Naye Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje alisema kuwa, kuhusu suala la Wachimbaji wadogo wa madini kutengewa maeneo ya uchimbaji, Wizara ya Nishati na Madini imebainisha eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 7.69 katika kijiji cha Kewanja wilayani Tarime ambalo linaweza kutoa leseni ndogo za uchimbaji madini zipatazo 76.

“ Aidha kuna maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji Wadogo kama eneo la Ilujamate wilayani Misungwi lenye ukubwa wa hekta 147, eneo la Nyangarata wilayani Kahama lenye hekta 1074 na eneo la Ibogelo mkoani Tabora lenye hekta 6,527 hivyo tunashauri wachimbaji wadogo wa madini wajitokeze katika kuomba maeneo hayo ya uchimbaji,” alisema Mhandisi Samaje.

No comments:

Post a Comment