Afisa Uwekezaji Mkuu kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Anitha Ishengoma (kushoto) akizungumza na vyombo vya habari kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Wananchi mbalimbali wakiangalia vipeperushi katika banda la Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Uchenjuaji Madini kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Priscus Kaspana (katikati) akionesha kipande cha mwamba na kutoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda hilo, kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
———————————————
Na Greyson Mwase
Imeelezwa kuwa Megawati 200 za umeme unaotokana na jotoardhi nchini zinatarajiwa kuzalishwa ifikapo mwaka 2025 na kumaliza changamoto ya ukosefu wa umeme nchini.
Hayo yameelezwa na Meneja Katika Masuala ya Sheria na Ukatibu kutoka Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Nchini (TGDC), Mershil Kivuyo katika maonesho ya kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akielezea mikakati ya kampuni hiyo, Kivuyo alisema kuwa mpaka sasa maeneo zaidi ya 50 yenye viashiria vya jotoardhi nchini yamegunduliwa ambayo kwa sasa yanafanyiwa kazi.
Alisema kuwa kampuni imeweka kipaumbele katika maeneo ya Ngozi na Songwe mkoani Mbeya, Luhoi mkoani Pwani, Kisaki mkoani Morogoro na Mount Meru mkoani Arusha.
Aliongeza kuwa utafiti wa kina umefanyika Ziwa Ngozi ambapo inatarajiwa kuchimbwa visima virefu mwaka 2017.
Akielezea manufaa ya Jotoardhi Kivuyo alieleza kuwa nishati ya jotoardhi itatumika kuzalisha umeme wa uhakika na hivyo kumaliza changamoto ya ukosefu wa umeme na hivyo kuongeza uwekezaji kwenye viwanda.
Aliongeza matumizi mengine kuwa ni pamoja na kukaushia mazao, kilimo cha maua na katika utengenezaji wa mabwawa.
Alisisitiza kuwa wawekezaji wanakaribishwa kwenye uwekezaji wa jotoardhi na kuchangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment